Sensa ya Idadi ya Watu na Makazi ya mwaka 2002 ilionyesha kwamba 
idadi ya watu
Tanzania iliongezeka kutoka milioni 23.1 mnamo 1988 hadi milioni 34.4 mnamo
2002, ikiwa ni wastani wa kiwango cha ukuaji cha asilimia 2.9 kwa mwaka. Sehemu ya watu wenye umri chini ya miaka 15 ilikuwa karibu asilimia 44, wakati wale 
wenye umri wa miaka 65 na zaidi walikuwa asilimia 4;ikionyesha kwamba Tanzania ina watu wengi vijana.
Muundo huu wa kuwepo watu wengi vijana una maana yaukuaji mkubwa wa idadi ya watu katika siku zijazo, 
pale vijana wanapoingia katika maisha yao ya uzazi bila 
kutilia maanani kama uwezo wa kuzaa unapungua au la.




Makisio ya idadi ya watu yanaonyesha kwamba 

Tanzania ina idadi ya watu milioni 37.9 mnamo 2006, na inatarajiwa kufikia milioni 63.5 mwaka 2025.

Sifa muhimu ya maelezo ya idadi ya watu ni msambao wake ndani ya nchi.
Uchanganuzi wa msambao wa idadi ya watu kimkoa uliofanywa katika sensa zote zilizopita 
unaonyesha kuwa karibu theluthi mbili ya watu iko katika robo ya nchi.

Kwa mujibu wa Sensa ya Idadi ya Watu na Makazi ya mwaka 2002, 

msambao wa watu hutofautiana kimkoa ambapo upo 
kati ya watu 12 kwa kilomita moja ya mraba kwa mkoa wa Lindi, 
hadi watu 1,700 kwa kilomita moja ya mraba kwa mkoa wa Mjini Magharibi (Zanzibar),na hadi kufikia kiwango cha juu cha watu 1,793 kwa
kilometa moja za mraba kwa mkoa wa Dar es Salaam. 

Sehemu kubwa ya idadi ya watu (asilimia 77 ya Watanzania wote) bado
wanaishi vijijini. Hata hivyo, idadi ya watu mijini imekuwa ikikua kwa kasi kwa zaidi ya asilimia 5 kwa mwaka katika Miongo mitatu iliyopita. 
Ukuaji huu wa kasi umesababishwa na uhamaji wa watu kutoka vijijini kwenda mijini kuliko kwa kipengele kingine chochote



CHANZO:SERA YA TAIFA YA IDADI YA WATU,
WIZARA YA MIPANGO, UCHUMI NA UWEZESHAJI (2006)
|