Pori la Akiba la hifadhi ya Taifa lililogeuzwa msitu mateso, mauaji Joseph Zablon
WENGI wamezoea kuuita Msitu wa Pande, lakini eneo hilo ni Pori la Akiba, lililopo kilometa 25 kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam katika Barabara Kuu kuelekea mji wa Bagamoyo.
Pori hilo la Akiba linamilikiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, lilitangazwa kuwa la akiba mwaka 1952.
Ili kufika Msitu wa Pande kutokea katikati ya mji, utalazimika kuteremkia kituo cha daladala cha Bunju ‘B’.
Kutoka hapo kuna daladala zisizo rasmi na pikipiki (bodaboda), ambazo zinasafirisha abiria kwa kutumia barabara inayoanzia eneo hilo kupitia katikati ya msitu huo hadi eneo la Mbezi, Barabara Kuu ya Morogoro.
Pori hilo lina ukubwa wa ekari 1,226 na kilometa za mraba 15.
Lilipewa hadhi ya kuwa Pori la Akiba baada ya kuzingatia vigezo mbalimbali na tafiti tofauti kubaini kuwepo kwa viumbe hai na aina za mimea adimu, zisizopatikana maeneo mengine.
Msitu wa Pande unazungukwa na vitongoji vya Mpiji Magohe, Kibesa, Msakuzi na Mbopo.
Hata hivyo, katika miaka ya karibuni pori hilo limejipatia sifa mbaya ya kutumika kama kichaka cha kutesea watu, mauaji na vituko mbalimbali.
Sifa hiyo mbaya ya pori hilo ilianza kuvuma mwaka 2006 baada ya wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, mkoani Morogoro kuuawa na polisi katika eneo hilo kwa kilichoelezwa kuwa walidhaniwa kuwa ni majambazi.
Baada ya hapo Tume iliundwa kuchunguza tukio hilo, ikabainika kuwa waliouawa hawakuwa majambazi.
Askari waliohusika na maujai hayo walifunguliwa kesi, ambayo ilivuta hisia za wengi kutokana na unyeti wake na mazingira ya tukio lenyewe.
Mbali ya vituko vya hapa na pale vinavyoshuhudiwa na kusimuliwa na majirani wa msitu huo, mwaka huu ikiwa miaka sita tangu kuuawa wafanyabiashara wa Mahenge, pori hilo limezizima tena, baada ya kiongozi wa madaktari, Dk Steven Ulimboka kutekwa, kuteswa na kisha kutelekezwa katika msitu huo.