KITABU kinachozungumzia kashfa ya kihistoria ya ununuzi wa rada, uliowahusisha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT) Dk. Idriss Rashidi, tayari kimeingia nchini.

Ndani ya kitabu hicho, kilichokuwa kikusubiriwa na wengi kiingie nchini, kinachoitwa The Shadow World Inside The Global Armrs Trade, Mtunzi Andrew Feinstein ameeleza kwa kina mchakato ulivyoendeshwa, ukiwahusisha watu wa madaraka na kada mbalimbali ambao ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.


Kitabu cha kashfa ya Rada na mtunzi wake

Andrew Feinstein

Tony Blair anatajwa katika kitabu hicho kuwa ndiye aliyemshawishi aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Benjamin Mkapa, kununua rada hiyo kutoka kampuni ya kutengeneza silaha ya Uingereza BAE-Systems.

Tanil Somaiya

Sailesh (Shailesh) Vithlani

Pamoja na hao, wanatajwa wafanyabiashara wenye asili ya India, lakini ambao wanaishi/walipata kuishi Tanzania, Tanil Somaiya ambaye alikuwa akimiliki kampuni ya uwakala wa simu ya Shivacom na Sailesh (Shailesh) Vithlani, kuwa watu wa kati wa biashara hiyo.Kuibuka kwa kitabu hicho kunaongezea tu katika taarifa za awali zilizopata kuchapishwa na kutangazwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini kuhusu ununuzi wa rada hiyo ambao ulipingwa sana si tu ndani ya Tanzania, bali hata Benki ya Dunia na Uingereza kwenyewe.

Wakati huo aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa, Clare Short, alikataa katakata Tanzania, moja kati ya nchi masikini kabisa duniani, kutumia mabilioni ya fedha kununua rada katikati ya umasikini unaonuka.

Anasema mwandishi wa kitabu hicho katika sehemu moja ya maandishi yake: “Wakati akipigia chapuo, Tume yake ya Afrika (Commission for Africa) juu malengo ya kuwa na utawala bora katika Afrika, Tony Blair alimshawishi Rais wa Tanzania, moja ya nchi masikini kabisa duniani kununua rada ya kijeshi kwa bei ya zaidi ya dola za Marekani milioni 40.

Wakati huo Tanzania ilikuwa na ndege nane tu za kivita, nyingi zikiwa katika hali mbovu kiasi cha kuzifanya zisitengenezeke. Rushwa ya karibu dola za Marekani milioni 10 inadaiwa ililipwa kwenye mpango huo.”

Kwa mujibu Andrew Feinstein, akiba ya dhahabu iliyohifadhiwa katika BoT ambayo, hata hivyo, thamani yake halisi haijafahamika, ndiyo iliyotumika kufadhili upatikanaji wa mabilioni ya fedha kwa njia ya mkopo kutoka Benki ya Barclays, ili kufanikisha ununuzi wenye utata wa rada ya kijeshi.

Katika taratibu za benki kuu mbalimbali duniani, dhahabu imekuwa ikihifadhiwa kama moja ya njia za nchi husika kujimudu dhidi ya mitikisiko ya kiuchumi. Tanzania ni kati ya nchi inayotumia mfumo huo wa kuhifadhi dhahabu.

Mwandishi huyo anasema katika kitabu hicho kwamba Dk. Idriss ndiye aliyekuwa kiungo muhimu katika kufanikisha mkopo kutoka Benki ya Barclays kwa masharti kuwa dhamana iwe akiba ya dhahabu iliyoko katika Benki Kuu ya Tanzania.

Bila kutaja thamani halisi ya akiba hiyo lakini akitaja kiwango cha mkopo husika, Andrew Feinstein anasema: “Katika mchakato huo, Dk. Idriss ndiye aliyekuwa na jukumu la kuidhinisha malipo hayo ya ununuzi wa rada (akiwa Gavana wa Benki Kuu), kwa masharti kwamba Benki ya Tanzania iweke dhamana akiba yake ya dhahabu ili mkopo (wa ununuzi rada) upatikane.

Feinstein anaeleza pia kwamba bosi huyo wa BoT ndiye aliyehakikisha michakato yote ya kifedha (malipo) inafanyika kwa mujibu wa sheria za Uingereza (zenye kinga katika michezo ya utoaji ‘chochote’ katika masuala ya ununuzi) na si sheria za Tanzania.

Mwandishi anasema Chenge, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, anatajwa kuhusika kutoa ushauri wa kisheria (kwa wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu), ushauri ambao unatajwa kuzingatiwa katika hatua nyingine za uamuzi, ukiwamo uamuzi wa Benki ya Barclays kutoa mkopo wa ununuzi wa rada.

Inadaiwa kuwa ili kuhakikisha mkopo kwa ajili ya ununuzi wa rada unapatikana kutoka Benki ya Barclays, wakala wa ununuzi huo Sailesh Vithlani, aliwasilisha nakala ya maoni ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzania (Chenge) katika Benki hiyo.


Andrew Chenge

Andrew Chenge

“Malipo yaliyofanywa kwenye akaunti ya Chenge yanalingana kikamilifu na uwasilishaji wa maoni yake (ya kisheria) kwa ajili ya kufanikisha upatikanaji wa mkopo na ununuzi wa rada.”

Kwa mujibu wa kitabu hicho, mazingira hayo ya ushiriki wa Chenge kwa njia ya kutoa ushauri wa kisheria yanathibitishwa na mawakili wake wa kimataifa, walioko Marekani pamoja na Uingereza ambao baada ya kuhojiwa walikiri ushiriki huo wa Chenge.

Namna walivyochota mamilioni

Inaelezwa kuwa kwa mujibu wa rasimu ya ripoti ya SFO (Taasisi ya Uchunguzi Makosa ya Jinai ya Uingereza), Chenge alipokea malipo ya jumla ya dola za Marekani milioni 1.5 (zaidi ya bilioni 1.5) kati ya Juni 1997 na Aprili 1998 kutoka Benki ya Barclays, tawi la Frankfurt.

Fedha hizo zililipwa katika benki ya Barclays huko Jersey - Uingereza, katika akaunti inayomilikiwa na kampuni iliyotajwa kwa jina la Franton Investment Limited. Kampuni hiyo imetajwa kumilikiwa na Chenge, ikiwa ni maalumu kwa ajili ya uhamishaji fedha kiasi cha dola za Marekani 600,000 (zaidi ya Sh milioni 600).

Maelezo zaidi katika kitabu hicho yanabainisha kuwa, dola hizo 600,000 za Marekani zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya kampuni ya Chenge kwenda kwenye akaunti nyingine, inayomilikiwa na Kampuni ya Langley Investments Ltd, iliyokuwa ikiendeshwa na Dk. Idrissa Rashidi (aliyewahi pia kuwa Mkurugenzi wa TANESCO).

Katika kitabu hicho, Feinstein ambaye aliwahoji washiriki mbalimbali wa sakata hilo, wakiwamo baadhi ya maofisa wa upelelezi nchini anasema: “Septemba 20, mwaka 1999, Chenge binafsi aliidhinisha uhamishaji wa dola za Marekani milioni 1.2 (zaidi ya Sh bilioni 1.2) kutoka akaunti ya kampuni (yake) ya Franton kwenda Royal Bank of Scotland International, huko Jersey.

Namna BAE ilivyojipenyeza

Mwaka 1997, kampuni ya BAE ilinunua kampuni iliyojulikana kama Siemens Plessey Systems (SPS) ambayo ilikuwa katika mchakato wa mapatano ya kibiashara na Serikali ya Tanzania tangu mwaka 1992 kwa ajili ya mauzo ya rada.

Kama sehemu ya makubaliano katika kuinunua kampuni ya Siemens Plessey Systems (SPS), BAE ilikubali kuendelea kumtumia wakala wa SPS, Sailesh (au Shailesh) Vithlani. Katika mazingira hayo, Sailesh aliomba kufanyike marekebisho kuhusu ahadi zake kwa maofisa wa Serikali ya Tanzania.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, ‘dili’ la mwanzo ambalo lingefanikisha biashara ya pauni za Uingereza milioni 110 lilizuiwa na Benki ya Dunia pamoja na Chombo mahsusi cha Uingereza cha kusimamia masuala ya maendeleo (Uk’s overseas Development Administration).

Uingiliaji wa Waziri Clare Short

Mwaka 2000, dili ikaibuka upya na safari hii kampuni ya BAE ikiligawa mradi (dili) huo katika awamu mbili ili kuunfanya uonekane ni mradi nafuu, lakini Clare Short, aliyepata kuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa alipinga mpango huo.

Upinzani huo ulihusisha hoja mbalimbali ambazo ni pamoja na mchakato mzima wa ununuzi umegubikwa na utata na kubwa zaidi, teknolojia ya rada hiyo imekwishapitwa na wakati. Hoja nyingine ni kwamba, Tanzania haina na shida na rada hiyo na badala yake, kilichokuwa kikihitajika ni rada ya ‘kiraia’ kwa ajili ya kuboresha huduma za anga na hasa kwa kuitazama sekta ya utalii.

Hata hivyo, licha ya upinzani wote huo kutoka kwa Waziri Clare Short na Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Uingereza kwa wakati huo, Robin Cook, mpango wa ununuzi wa rada uliendelea mwaka 2001 kwa BAE System kuiuzia Tanzania rada kwa thamani ya pauni za Uingereza milioni 28.

Katika hali ya kupinga mchakato wa ununuzi wa rada hiyo, Oktoba, mwaka 2001 ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya Usalama wa Anga (ICAO), ilieleza kasoro katika ununuzi wa rada hiyo ya kijeshi.

Ripoti hiyo inanukuliwa ikisema; “Rada inayonunuliwa ni kwa ajili ya shughuli za kijeshi na kwa hiyo, haitakuwa na msaada mkubwa kwa shughuli za anga kwa ajili ya ndege za kiraia. Mpango wa ununuzi wa rada hiyo si sahihi na ni wa gharama mno.”

Kutokana na ripoti hiyo, Kampuni ya BAE iliishushia lawama ICAO kwamba imetoa taarifa za uongo na hasa kwa upande wa gharama za uuzaji.

Lakini wakati BAE na ICAO wakiingia katika malumbano, Msemaji wa Benki ya Dunia alitoa tamko akisema; “Matumizi hayo ya fedha (ununuzi) hayako wazi, yana utata mkubwa.”

Tafsiri iliyotolewa ni kwamba, bajeti ya dola za Marekani milioni 40 kwa ajili ya ununuzi wa rada hiyo ni sawa na theluthi moja ya bajeti ya elimu nchini Tanzania na kwa hiyo, ni kiwango kikubwa cha fedha ambacho kinakinzana na vipaumbele vya kibajeti vya Tanzania, kama elimu na afya.

Wengi walipata kuzungumzia sakata hilo la ununuzi wa rada wa karibuni kabisa akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye alisema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba angezungmzia suala hilo kwa kutaja wahusika wakati wa kuwasilisha bajeti ya wizara yake akijibu hoja za wabunge waliokuwa wanataka wahusika watajwe hadharani na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Huko nyuma Chenge mwenyewe alipata kuzungumzia suala hilo, na hasa, kumiliki kwake kwa akaunti za fedha nyingi nje ya nchi yeye akiwa kama mtumishi wa umma.

Akiwajibu waandishi wa habari wakati wa safari yake moja ya kurejea nchini, Chenge alisema fedha hizo zilikuwa ni vijisenti tu, kauli ambayo iliwatibua wengi wa Watanzania ambao shilingi kwao ilikuwa imeota matairi.

Na katika hatua nyingine wakati huo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Edward Hosea alipata, mara mbili, kunukuliwa akisema Chenge hakuwa na kesi ya kujibu katika kashfa hiyo ya rada.

Kitabu hiki kimetua nchini katikati ya taarifa za ufisadi mwingine uliofanywa na Watanzania, wakiwamo wastaafu wa vyeo vya juu wanaotajwa kuwa wamefutika fedha zinazokadiriwa kuwa mabilioni ya shilingi katika akaunti za nchini Uswisi zinazotokana na migao ya rushwa.

Thanks to Gazeti la Raia Mwema na Uchambuzi makini

|
0 Responses